Chadema kuitisha maandamano nchi nzima


Chadema kuitisha maandamano nchi nzima


Wamwandikia barua JK awawajibishe vigogo
*Waishukia TBC, wataka wananchi wasiiangalie, wasipeleke matangazo
*Madiwani wawili Mwanza wavuliwa uanachama

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kitaiti sha maandamano ya kihistoria nchi nzima, kupinga unyanyasaji unaofanywa na Jeshi la Polisi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliwambia waandishi wa habari jana mjini Dar es Salaam kuwa, maandamano hayo yatakuwa makubwa na yataingia katika kumbukumbu za nchi hii. 

Kwa mujibu wa Mbowe, maandamano hayo ambayo yatafanyika wakati wowote, yanalenga kuwashinikiza baadhi ya viongozi wajiuzulu kwa kile kinachoelezwa kuwa, wameshindwa kutimiza wajibu wao.

Mbowe aliwataja wanaolengwa wakati wa maandamano hayo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna Paul Changoja, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile pamoja na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.

Wengine ni Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa na makamanda wa vikosi vya kutuliza ghasia wa Mikoa ya Arusha, Morogoro, Iringa na Singida.

Katika mazungumzo yake, Mbowe alisema maazimio hayo yalitolewa na Kamati Kuu ya chama hicho iliyokaa juzi jijini Dar es Salaam.

“Kamati Kuu imezingatia masuala mbalimbali na kupitisha maazimio nane na tayari tumemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete, ili awachukulie hatua viongozi hao tuliowataja.

“Iwapo Serikali haitazingatia kutekeleza maamuzi na mapendekezo ya Kamati Kuu na kuyapuuza kama ilivyo kawaida yao, CHADEMA itawaongoza wananchi kwa njia za demokrasia ikiwamo maandamano ya amani ya nchi nzima, kushinikiza hatua za haraka dhidi ya viongozi hao kwa maslahi ya taifa.

“Kuna mfumo au mazoea kwa Jeshi la Polisi kutangulizwa kuzuia maandamano, safari hii maandamano hayo yatakuwa ya historia tangu tupate uhuru, naombeni polisi sambamba na Jeshi letu la Ulinzi, wajiandae vya kutosha ingawa najua hawataweza,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema, viongozi wanaotakiwa kujiuzulu wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwamo za mauaji kwa raia wasio na hatia katika maeneo ya Arusha, Igunga, Arumeru Mashariki, Singida, Morogoro na Iringa.

“Tunamuomba Rais Kikwete kama viongozi hao watashindwa kujiuzulu wenyewe kabla sisi CHADEMA hatujachukua hatua dhidi yao, ni vema aokoe jahazi hili kwa kuwavua madaraka kwa sababu mauaji yote ya raia yametokea mikononi mwa Jeshi la Polisi,” alisema na kuongeza.

CHADEMA haitatangaza siku ya maandamano hayo ya nchi nzima, kwa sababu tukitangaza sasa hivi polisi watajiandaa kutudhibiti kama ilivyo kawaida yao.

“Siku wala muda hautatangazwa hiyo ni siri yetu, najua kuna maswali mengi juu ya tukio hili, lakini nawaambieni tutatumia njia zozote hata kwa ungo tutasambaa nchi nzima,” alisema Mbowe.

Katika hatua nyingine, alisema Rais Kikwete anatakiwa kuunda tume huru, ili kuchunguza vifo vilivyotokea katika mazingira ya kutatanisha chini ya Jeshi la Polisi.

“Kumekuwa na ushirikiano haramu baina ya Serikali, CCM na Jeshi la Polisi katika kudhibiti Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), ambapo baadhi ya wananchi wanapoteza maisha.

“Kwa hiyo, sasa wakati umefika wa kuwadhibiti na kuwawajibisha viongozi wetu na njia hiyo ni ya maandamano, kwani wameshindwa kufuata na kuziheshimu sheria zilizopo na ndio maana mnamuona Tendwa akitoa kauli tata zenye mwelekeo wa kuibeba CCM na Serikali. 

“Hivyo basi, Tendwa hafai kuendelea kushikilia nafasi hiyo na tunatangaza rasmi hatutakuwa na ushirikiano na ofisi yake, hadi hapo atakapowekwa msajili mwingine.

“Kauli ya kusema atakifuta CHADEMA, anajidanganya mwenyewe, hakuna anayeweza kukifuta chama hiki kwa muda huu, hata kama wataagizwa na Rais Kikwete, kama wanajiamini wajaribu waone moto utakaowaka,” alijigamba Mbowe.

TAMKO KWA TBC

Akizungumzia vyombo vya habari, alisema chama chake kinashangazwa na mwenendo wa Televisheni ya Taifa (TBC), ambayo imekuwa ikipotosha habari za CHADEMA.

“Vyombo vya habari vya umma hususan TBC, vimeendelea kuripoti taarifa zenye mwelekeo wa kipropaganda kwa kutumiwa kwa manufaa ya CCM, ili kupotosha ukweli wa mambo na matukio mbalimbali ya siasa yanayotokea nchini.

“TBC imekuwa ikipotosha ukweli kuhusu shughuli za kisiasa zinazofanywa na CHADEMA, kwa hiyo, Kamati Kuu imeamua kutangaza mgogoro rasmi na TBC, ambapo tunawaomba Watanzania wasusie TBC na vyombo vingine vya Serikali.

“Tunatambua vyombo vya umma vinaendeshwa kwa kodi za wananchi na vinapashwa kuripoti taarifa zao bila upendeleo wowote na kwa weledi, maadili na utalaamu wa hali ya juu.

“Kwa kuwa TBC na vyombo vingine vya Serikali wameshindwa kufanya hivyo kwa kufuata maadili, Kamati Kuu inatoa wito kwa wanachama na wananchi wote wapenda mabadiliko, kuvisusia vyombo hivyo kwa kutoviangalia, kusikiliza na kutovipelekea matangazo hadi hapo vitakapojirekebisha.

CHADEMA kuanzia leo, tunatarajia kuanzisha kampeni ya kuwaeleza Watanzania wote juu ya mwenendo wa TBC na jinsi inavyotumia kodi zao kulinda maslahi ya CCM na viongozi wao ambao asilimia kubwa wanajihusisha na wizi, ufisadi na mauaji.

“TBC imekuwa adui wa haki na ukweli katika taifa hili na imebeba taswira ya kipropaganda za CCM, jambo ambalo ni hatari kwa amani na mshikamno wa kitaifa,” alisema Mbowe.

MADIWANI MWANZA WAVULIWA UANACHAMA

Katika hatua nyingine, Mbowe alisema Kamati Kuu ilipokea taarifa ya Kamati Ndogo iliyoundwa na Katibu Mkuu wao, Dk. Willbrod Slaa kuchunguza mgogoro wa chama hicho mkoani Mwanza.

Baada ya kujadili taarifa hiyo, alisema kamati hiyo imeamua kuwavua uanachama madiwani wawili wa chama hicho, Adams Chagulani wa Kata ya Igoma na Henry Matata wa Kata ya Kitangiri.

Alisema kwamba, madiwani hao walikiuka Katiba ya CHADEMA, kanuni na maadili ya chama hicho, kwa kujihusisha na tuhuma za ufisadi, ambapo walijihusisha na mbinu chafu za CCM kumg’oa Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere kwa lengo la kuidhoofisha CHADEMA

Kwa mujibu wa Mbowe, madiwani hao kabla ya kuchukuliwa hatua, walipewa onyo lakini hawakutaka kubadilika kutokana na sababu wanazozijua wao.

Alisema kutokana na hali hiyo kamati hiyo imeamua kuvunja uongozi wote wa Mwanza wa chama chao, kutokana na kushindwa kuwajibika vizuri na kuruhusu vitendo vya kihuni kufanyika kwa ufadhili wa CCM.

Kutokana na hali hiyo, alisema CHADEMA ipo tayari kuingia kwenye uchaguzi wa madiwani, kwa sababu lengo ni kuimarisha uongozi wa chama chao.

M4C KUANZA TENA

Wakati huo huo, Mbowe alitangaza kuanza kwa operesheni ya mikutano ya M4C katika Mikoa ya Iringa na Singida, huku akisema kwamba amepania kufika katika Jimbo la Singida Magharibi, linaloongozwa na Mwigulu Nchemba ambaye anajidai ni bingwa wa propaganda.

Alisema katika jimbo hilo atahakikisha anafanya mikutano mitaa yote ya jimbo, huku akimtahadharisha kutoingilia mikutano yake.

Wakati Mbowe akisema hayo, juzi CHADEMA walionyesha kwa waandishi wa habari picha za video zinazoonyesha jinsi Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi alivyouawa.

Katika picha hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alionekana akishuhudia Mwangosi akiuawa.


Comments

Popular posts from this blog

VARIOUS MASONIC SYMBOLS

CHADEMA yazidi kuikalia kooni CCM

KANUMBA THE GREATS