waziri mkuu Mizengo Pinda aihofia chadema



Pinda aihofia CHADEMA

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiko jirani na Chama cha Mapinduzi (CCM). Pinda alitoa kauli hiyo juzi wilayani hapa kabla ya kuanza ziara yake katika Vijiji vya Bugulula na Senga wilayani Geita kwa ajili ya kuzindua miradi ya maendeleo.

Katika kijiji cha Bugulula, Waziri Mkuu alizindua mradi wa ufugaji wa kisasa wa nyuki na Senga alifungua jengo la kliniki ya baba, mama na watoto. 

Wakati Waziri Mkuu akitoa kauli hiyo, alikuwa akimtambulisha Mbunge wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi (CHADEMA).

Baada ya kauli hiyo, baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali walionekana kucheka.

“Mkuu wa Mkoa, ngoja, ngoja kwanza, Profesa Kahigi hebu simama, unajua wengi hawakujui, ndugu zangu, huyu hapa (Profesa Kahigi) ni Mbunge mwenzangu ingawa yeyé yuko Jimbo la Bukombe, kupitia kile chama kilicho jirani yetu.

“Hamuwezi kuamini, pamoja na kwamba ni Mbunge kupitia hiki chama kilicho jirani yetu, ninachotaka kusema ni kwamba huyu ni rafiki yangu mkubwa, tena naweza kusema hakuna rafiki yangu mkubwa kama ilivyo kwa Profesa Kahigi,”alisema Waziri Mkuu Pinda na kusababisha viongozi wote waliokuwa eneo hilo kuvunjika mbavu kwa kicheko.

Awali, akizungumza mjini hapa, Pinda alisema, migogoro ya wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu dhidi ya wawekezaji wakubwa, haitakwisha kama hawatatengewa maeneo ya kuruhusu kufanya shughuli za uchimbaji.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja kwa wawekezaji wakubwa kukubali kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo ambao wamekuwa wakidaiwa kuvamia baadhi ya maeneo ya migodi kwa ajili ya kujitafutia maisha.

Alisema, migogoro inayotokea sasa inajenga uhusiano mbaya kwa wachimbaji wadogo na wakubwa na jamii inayozunguka maeneo hayo.

"Suala hili la migogoro ya wawekezaji wakubwa dhidi ya wachimbaji wazalendo wadogo haliwezi kwisha kama wamiliki wa migodi mikubwa hawatakuwa tayari kukubali kuwatengea walau maeneo kidogo wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba na kujipatia mahitaji yao,"alisema Pinda.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu Pinda aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omary Mangochie iliyoonyesha, moja ya changamoto kubwa katika wilaya hiyo ni ongezeko la migogoro ya wachimbaji wadogo dhidi ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).

Aliwasihi viongozi wa GGM kukubali kutenga maeneo machache ili wachimbaji wadogo waweze kupata maeneo kwa ajili yao badala ya kuendelea kuwa na mvutano ambao umekuwa chanzo cha baadhi ya wananchi kupoteza maisha kutokana na kuvamia kwenye maeneo ya mgodi huo.

"Bahati nzuri leo tumejaliwa kuwa na viongozi wa Mgodi wa GGM, niwaombe ndugu zangu mkubali kutenga walau maeneo kidogo ambayo hamjaanza kuyachimba kutoka kwenye maeneo yenu mnayoyamiliki kwa lengo la kupunguza migogoro isiyo ya lazima na wachimbaji hawa wadogo,"alisema Waziri Mkuu Pinda.

Kuhusu mabaki ya miamba, alisema Serikali inatarajia kuzungumza na wawekezaji hao ili kuweka utaratibu mzuri wa kuyakusanya kwenye maeneo maalumu ili iwe rahisi kwa wananchi kufika na kuyachukua kwa ajili ya kwenda kusaga na kutafuta mabaki ya dhahabu

Comments

Popular posts from this blog

VARIOUS MASONIC SYMBOLS

CHADEMA yazidi kuikalia kooni CCM

KANUMBA THE GREATS